Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu 2014






Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso- Boiano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya matatizo ya kijamii, kazi, haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ndiye aliyepewa dhamana ya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu tarehe 18 Aprili 2014 Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia saa 3:15 Usiku kwa majira ya Ulaya, baadaye atatoa baraka zake za kitume. RealAudioMP3

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa ufupi, tafakari ya Njia ya Msalaba iliyoandaliwa na Askofu mkuu Bregantini.

Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua kuwa anasema ukweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana haya yalitukia ili andiko litimie: hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: watamtazama yeye waliyemchoma. Hivi ndivyo Askofu mkuu Bregantini anavyoanza tafakari ya Njia ya Msalaba, kwa kuonesha kwamba, Yesu alipanda kwenda Mlimani Golgota bila kusita, kama kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa na akawaruhusu watesi wake kumtendea jeuri bila kulalama!

Yesu, Mwana wa Maria alipenda kubeba mabegani mwake, matendo ya giza yanayomwandama mwanadamu katika hija yake ya maisha, ili kuweza kumkirimia mwanga, unaoleta nuru katika moyo wake. Mateso na mahangaiko ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu; machozi yake yanaonesha upendo wa Mungu. Yesu amesamehe dhambi za binadamu ili kwa njia ya maisha yake, aweze kuwaonesha njia ya wokovu kutokana na mateso pamoja na mahangaiko wanayokabiliana nayo katika maisha, pasi na kukata tamaa.

Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anajisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya wadhambi ambao kwa haki kabisa walistahili kutundikwa pale juu Msalabani. Kiu inayooneshwa na Yesu pale Msalabani ni chemchemi ya matumaini yaliyo wazi na mikono iliyo tayari kumpokea mdhambi anayetubu na kumwongokea Mungu. Askofu mkuu Bregantini anamwomba Yesu Msulubiwa kuwakirimia watu huruma yake isiyokuwa na kifani, kwa kuwaonjesha harufu nzuri iliyoujaza mji wa Bethania, mwanzo wa maisha mapya. Kwa kifo cha Kristo Msalabani, Yesu awajalie waamini maisha ya uzima wa milele.

Katika tafakari yake, Askofu mkuu Bregantini anagusia mashitaka yanayoendelea kujitokeza ulimwenguni kwa kujikita katika ubaguzi wa rangi, hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, kielelezo cha dhamiri mfu, inayoonesha jinsi watu wanavyoshindwa kuwajibika na ukweli kutawala, changamoto ya kusimama kidete kutetea wanyonge na kulinda ukweli.

Msalaba wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa unazidi kuwaelemea watu wengi kwa kukosa fursa za ajira, mshikamano wa upendo na udugu; matumaini na imani thabiti. Msalaba unaweza kuwa rahisi, ikiwa kama watu watajifunza kuubeba pamoja na Yes una kwamba, kwa njia ya udhaifu wa kibinadamu, watu wajifunze kujenga na kudumisha moyo wa ukarimu, kwani sura ya wote wanaoteseka, inaonesha pia ile sura ya Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake.

Kuna akina Mama na wanawake wanaoendelea kuwalilia watoto wao wanaofariki dunia kutokana na sababu mbali mbali; watoto kupelekwa mstari wa mbele vitani; watoto wanaofariki kwa saratani kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira; watoto wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Kwa kushikamana na Bikira Maria, hakuna hata chozi moja linaweza kupotea, kwani Bikira Maria ni Mama wa wote.

Kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa kuguswa na mateso na mahangaiko ya jirani, daima lengo likiwa ni kutafuta mafao na ustawi wa wengi, ili kushinda vikwazo vya chuki, uhasama na kuonea wivu. Tafakari ya Njia ya Msalaba inamwonesha Veronika, mwanamke mwenye huruma anayethubutu kupangusa uso wa Yesu na hivyo kushiriki katika mateso yake. Yesu anatambua upendo na ukarimu wa Veronika, changamoto ya kuguswa na wale wanaoishi katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia kifo!

Wafungwa ni kundi la watu wanaoendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa haki jamii na mifumo duni ya maisha kwa kuishi hata kinyume kabisa cha ubinadamu, hawa wanaendelea kuvikwa taji la miiba viwachani wao. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza watu wanaojitolea kutoa huduma mbali mbali za kiroho na kimwili kwa wafungwa gerezani.

Katika tafakari hii, wanawake wakweli na waaminifu wanaoneshwa wakimsindikiza Yesu katika Njia ya Msalaba, wanataka kumsalimia na kumfariji, changamoto ya kuendelea kuwa imara katika imani na matumaini; kwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Yesu anapoanguka mara kadhaa kwa kuelemewa na uzito wa Msalaba, anawalika waamini kujibidisha kushinda tabia chafu zinazowaangusha daima dhambini. Waamini wajenge umoja na mshikamano, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika upatanisho, kwa kuwamngalia Yesu anayetundikwa Msalabani.

Watu wajenge utamadni wa kuwaheshimu, kuwajali na kuwahudumia wagonjwa badala ya kuwatelekeza na kuwatafutia njia ya mkato ya kumaliza mahangaiko yao kwa kifo laini. Yesu hakushuka Msalabani, aliendelea kupenda na kusamehe. Ugonjwa unaweza kuwa ni shule ya hekima ya kimungu, mahali pa kukutana na Mungu mpole na mvumilivu, mwaliko wa kupambana na magonjwa katika mwanga wa Pasaka na mafao ya familia na Jamii kwa ujumla.

Maneno saba ya Yesu Msalabani ni chemchemi ya upendo na kwamba, kifo cha Kristo kinafungua ukurasa mpya kwa kuonesha kwamba, kifo hakina tena nguvu! Msamaha unaponya na kupyaisha; unawaunda watu katika maisha mapya, mwaliko wa kuondokana na falsafa ya vita, kwani upendo na mshikamano ni mambo yenye nguvu zaidi kuliko hata kifo! Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia huduma ya upendo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Fundisho kuu ambalo Yesu amewaachia wafuasi wake ni kupenda bila ya kujibakiza, ndiyo maana Bikira Maria anathubutu kupokea maiti ya mwanaye kwa imani na matumaini makubwa! Mwanadamu anakumbushwa kwamba, hapa duniani ni mpita njia, iko siku ataungana na Muumba wake. Katika kimya kikuu pale bustanini kulikokuwa na kaburi la Yesu, waamini wajitaabishe kusikiliza sauti ya Yesu ikisema, mimi niko pamoja nanyi hadi ukamilifu wa dahali.

Kwa ufupi, haya ndiyo mawazo makuu yanayochambuliwa na Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini katika tafakari yake ya Njia ya Msalaba, Ijumaa Kuu kuzunguka magofu ya Colosseo, mjini Roma.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.




0 Response to "Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu 2014 "